6 Oktoba 2020 - 11:32
Mufti Mkuu wa Oman akosoa vikali matamshi ya Rais wa Ufaransa dhidi ya Uislamu

Mufti Mkuu wa Oman Sheikh Ahmad Hamad al-Khalili amekosoa vikali matamshi ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kusema kuwa, matamshi hayo ni ya kichochezi na yanalenga kutafuta uungaji wa makundi yenye kufurutu ada katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mufti al-Khalili amebainisha kuwa, matamshi ya kichochezi ya Rais Macron yanalenga kutafuta uungaji wa makundi ya walio wachache yenye misimamo ya kufurutu ada nchini Ufaransa.

Mufti huyo wa Oman ameongeza kuwa, maadui wa Uislamu wangali wanavizia na wanatumia ndimi na kalamu zao kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu.

Sheikh Ahmad al-Khalili ameutaja Uislamu kuwa ni safina ya wokovu ambayo inauokoa na kuuepusha ulimwengu na kuzama.

Wanafikra na wasomi wote licha ya hitilafu zaio, lakini wameafikiana juu ya suala hili kwamba, utatuzi wa mataizo yote yanayoukabili ulimwenguu hii leo ni Uislamu, amesisitiza Mufti Mkuu wa Oman.

Aidha ameongeza kuwa, njama za kuunasibisha Uislamu na tuhuma zisizo na msingi hazitakuwa na natijaya maana kwa wale wanaotoa tuhuma hizo na watashindwa vibaya. 

Katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Emmanuel Macron hivi karibuni alizindua mpango wa kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kama "Misimamo Mikali ya Kiislamu". Rais wa Ufaransa alidai pia kuwa Uislamu ni dini iliyo "kwenye mgogoro" ulimwengu mzima.

Katika hotuba yake hiyo ambayo imewaudhi Waislamu wa maeneo mbalimbali ulimwenguni Macron alisema, serikali yake itawasilisha muswada mwezi Desemba wa kuimarisha sheria ya 1905 ya nchi hiyo ambayo ilitenganisha rasmi Kanisa na utawala.

342/